27 Septemba 2026 - 22:32
Hawza ya Hazrat Abul-Fadhil al-Abbas (a.s.) mjini Tanga |  Darsa ya Maadili ya Mtume (s.a.w.w.) Yasisitiza Uadilifu Kama Mfumo wa Maisha ya Mwanadamu

Darsa ya maadili iliyofanyika katika Msikiti na Hawza ya Hazrat Abul-Fadhil al-Abbas (a.s.) mjini Tanga imeeleza nafasi ya uadilifu katika mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.), huku ikisisitiza kuwa uadilifu haupaswi kubaki kuwa kauli ya kimaadili, bali unapaswa kuwa msingi wa maisha katika familia, jamii, biashara, uongozi na mahusiano ya wanadamu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s.) –ABNA–, darsa ya maadili ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) imefanyika katika Msikiti na Hawza ya Hazrat Abul-Fadhil al-Abbas (a.s.), mjini Tanga, Tanzania, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa shughuli za kidini, kielimu, kitamaduni na kitablighi zinazofanyika katika kituo hicho.

Darsa hiyo iliyofanyika tarehe 27 Septemba 2026, iliwasilishwa na Sheikh Shafi Nina, na ilijikita katika mada ya “Maadili ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na Uadilifu Kama Mfumo wa Maisha ya Mwanadamu.”

Msikiti na Hawza ya Hazrat Abul-Fadhil al-Abbas (a.s.) ni miongoni mwa vituo hai vya Kiislamu vilivyopo katika Jiji la Tanga, ambavyo vinafanya shughuli za kidini na kitablighi kwa kushirikiana na Uwakilishi wa Jamiat Al-Mustafa (s) nchini Tanzania. Kituo hicho kinajishughulisha na ufundishaji wa maarifa ya Kiislamu, shughuli za kiutamaduni, pamoja na programu za kitablighi na malezi, chini ya uongozi wa Sheikh Shafi Nina.

Akizungumza katika darsa hiyo, Sheikh Shafi Nina alieleza umuhimu wa maadili katika Sira na mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.), akilenga zaidi nafasi ya uadilifu kama moja ya misingi muhimu ya maisha ya mwanadamu.

Sheikh Shafi Nina alibainisha kuwa dhana ya uadilifu na tabia ya kutenda kwa haki ilikuwa ikijulikana miongoni mwa wanadamu hata kabla ya kutumwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kama mjumbe wa Allah. Hata hivyo, alisema kuwa kupitia risala ya Mtume (s.a.w.w.), uadilifu ulipewa nafasi pana zaidi na kuwa sehemu ya mfumo wa maisha ya mwanadamu.

Kwa mujibu wa maelezo yake, mafundisho ya Mtume (s.a.w.w.) hayakuweka uadilifu katika kiwango cha tabia binafsi pekee, bali yaliuhusisha na nyanja mbalimbali za maisha, ikiwemo familia, jamii, biashara, uongozi na mahusiano ya kibinadamu.

Katika kufafanua suala hilo, Sheikh Shafi Nina alisisitiza kuwa uadilifu haupaswi kuishia katika kuwatendea haki watu tunaowapenda au marafiki zetu pekee, bali unapaswa kuzingatiwa hata katika mahusiano na watu ambao tunatofautiana nao.

Miongoni mwa mifano ya uadilifu iliyotolewa katika darsa hiyo ni:

🔹 Katika mahusiano ya kijamii: Kumtendea haki si rafiki pekee, bali pia mtu ambaye hamkubaliani au hampendi.

🔹 Katika biashara: Kuepuka udanganyifu, kupunguza vipimo na mizani, pamoja na aina nyingine za ulaghai katika biashara na miamala.

🔹 Katika uongozi: Kuepuka upendeleo kwa ndugu, watu wenye mali au wenye nafasi maalumu, na kuhakikisha maamuzi yanazingatia haki.

🔹 Katika hukumu na uamuzi: Kutomdhulumu mtu kwa sababu ya kabila, dini, nafasi yake katika jamii au hali yake ya kijamii.

Kwa kumalizia, Sheikh Shafi Nina alieleza kuwa moja ya mafundisho muhimu ya maadili ya Mtume (s.a.w.w.) ni kwamba maadili kama uadilifu hayapaswi kubaki katika kiwango cha ushauri au maneno mazuri pekee, bali yanapaswa kugeuzwa kuwa kanuni za vitendo katika maisha ya kila siku.

Darsa hiyo ya maadili na mawaidha ya Kiislamu hufanyika kila wiki baada ya Sala ya Adhuhuri na Alasiri katika Msikiti na Hawza ya Hazrat Abul-Fadhil al-Abbas (a.s.), na hushirikisha wanafunzi wa Hawza, waumini pamoja na wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka kituo hicho.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha